Mwanzo > Habari Mpya za ubalozi wa China
Afrika Njia Panda: Matokeo ya Vita Baridi yajirudia katikati ya Mkakati mpya wa Marekani kuhusu Afrika
Francis Semwaza
2018-12-31 02:37

Uzinduzi wa Mkakati wa Marekani unaolenga Afrika unaleta changamoto mpya kabisa kwenye siasa za kimkakati za dunia, kwa kuzingatia kwamba siasa za chuki za nchi za Magharibi dhidi ya China zinazidi kujipambanua, hususan pale bara la Afrika linapohusika.

Ukipambanuliwa vema na nguli anayefahamika kwa msimamo mkali kwenye sera za mambo ya nje ambaye pia ni Mshauri wa Usalama wa Nchi hiyo, John Bolton, mkakati huo unaeleza nia ya kuanzisha mapambano na washindani wa Marekani huku mahitaji ya Waafrika na nchi zao yakisahauliwa.

Baada ya kuitaja China angalau mara 15 na nchi moja tu ya Kiafrika ambayo ni Sudan Kusini, ikitajwa zaidi, mara 5 tu, katika hotuba ya uzinduzi aliyoitoa Bolton, hali hii itafanya mtu yeyote ashangae iwapo kile kinachoitwa 'Mkakati wa Afrika' ni kweli unalenga kuinufaisha Afrika au kulichukulia bara hilo kama uwanja wa vita tu katika kukabiliana na China na Urusi!

Mbali na kuzilazimisha nchi kuchagua upande mmoja dhidi ya mwingine, na kukosoa mbinu zinazotumiwa na China barani Afrika kuwa zimegubikwa na rushwa, uamuzi wa Marekani kutumia fikra za kale katika mkakati wake barani Afrika umewaacha na maswali hata baadhi ya wasomi wake kwani umeshindwa kueleza namna ambavyo utatekelezwa. Katika masikio ya wengi, inaweza kuonekana kana kwamba huo ni mwendelezo wa mbinu ya ukoloni ya 'kugawa na kutawala' kuliko kuwa mpango halisi wa maendeleo.

Uzoefu unathibitisha kwamba, hiki ndicho kilichotokea wakati wa kipindi cha Vita Baridi  pale nchi kama Angola, Msumbiji, Afrika Kusini na nyinginezo zilitokwa na damu nyingi wakati wa siasa za kuunga mkono vita vya kiitikadi kati ya 'Mashariki' na 'Magharibi', dhana zilizowakilisha hadithi ya mapambano kati ya ubepari na ujamaa.

Kurejea kwa siasa za chuki dhidi ya China na Urusi barani Afrika kunaliweka bara hilo katika njiapanda ya namna ya kusitawisha na kuimarisha uhuru, amani na uimara wa nchi: hii ikiwa ni pamoja na kuweza kujikinga dhidi ya propaganda nyepesi za kupinga maendeleo, zikiwemo habari potofu kwamba China imeipora Kampuni ya Umeme ya Taifa ya Zambia, ZESCO, na ile ya kuporwa kwa bandari ya Mombasa nchini Kenya, ambazo zote ni utoposhaji mkubwa.

Sera hiyo mpya ya Marekani kwa Afrika inayoelezwa kuwa 'imechelewa', pia imekosolewa na baadhi ya watu mashuhuri akiwemo Mwenyekiti wa sasa wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Bw. Moussa Faki Mahamat, kama 'kuidumaza Afrika', akisisitiza kuwa Afrika iko huru kuchagua na kushirikiana na nchi yoyote kama marafiki zake.

Kujinasua katika mtego huo kunaweza kuwa kazi ya ngumu zaidi kwa Afrika kwa kuzingatia mfungamano na ukaribu uliopo kati ya nchi mbalimbali za Kiafrika na nchi zilizoendelea: hivyo basi, si ajabu kwa mfano kukuta nchi kama China, Canada, Urusi na Marekani zote kwa pamoja zikishiriki katika kuendeleza jeshi la nchi moja ya Afrika.

Kwa kupitia kivuli cha misaada, mataifa makubwa kadhaa ya kigeni yameweza kujipenyeza ndani kabisa, yaani kwenye kiini, cha jamii mbalimbali za Kiafrika, kiasi cha kuweza kushawishi masuala ya msingi kadiri wanavyoona inafaa kwa kuzingatia maslahi ya nchi zao: si ajabu kwamba wageni wengi wameweza kuifahamu zaidi Afrika kuliko ambavyo Waafrika wenyewe wanaifahamu.

Ni dhahiri kuwa nchi hizo zitakuwa zikitoa misada huku zikiwa na dhamira mbalimbali zinazodumisha maslahi yao, jaribio ambalo China imeweza kulivuka hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba imejikita katika kutoa misaada ya dhati kwa karne kadhaa sasa, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya msingi kama vile barabara, reli na kuendeleza bandari katika nchi kadhaa za Afrika tangu miaka ya 1960 hadi leo.

Kwa kuzingatia urefu wa muda na kiwango cha msaada ambacho kila nchi ya kigeni imesaidia katika sekta fulani, kusitisha mahusiano kabisa ni jambo lisilowezekana na hivyo kufanya utekelezaji wa Mkakati wa Marekani kwa Afrika kuwa mgumu, hususan pale linapokuja suala la kupewa maelekezo ya kuchagua kati ya nchi za Magharibi kwa upande mmoja, au China na Urusi kwa upande mwingine.

Ugumu wa kuchagua nchi 'rafiki' na 'adui' unaongezeka kutokana na kujipenyeza kwa nchi mbalimbali za kigeni hadi katika masuala ya ndani kabisa ya nchi za Afrika, na hivyo kufanya ndoto za Waasisi wa Mataifa yetu, ikiwemo ile ya kujitegemea, kuwa ngumu kutimizwa kwani haziwezi kupewa uzito unaostahili kama ilivyokuwa katika miaka michache baada ya kujipatia uhuru.

Pengine ingekuwa hekima kwa nchi yoyote ya Kiafrika inayohisi kunasa kwenye mtego wa aina hii kufuata hekima za Mzee Kwame Nkrumah aliposhauri 'kutokwenda Mashariki wala Magharibi,' na badala yake kusonga mbele katika kuboresha ustawi wa watu wa Afrika kupitia ushirikiano, misaada na sera za kirafiki ambazo zinalenga kuiendeleza Afrika, badala ya zile zinazotaka kutibua urafiki uliopo kati ya Afrika na marafiki zake wa kuaminika, ikiwemo China.

Hata hivyo, ingawa mwanzoni lugha inayotumika inaweza kuifanya hali ya mchuano kati ya nchi za Magharibi dhidi ya China na Urusi ifanane na hali ilivyokuwa wakati wa Vita Baridi, uhalisia unaweza kuwa mgumu zaidi kudadavua kuliko inavyofikiriwa, kwa sababu maslahi katika siasa za kimataifa si ya upande mmoja tena, bali yanaingiliana kati ya nchi na nchi.

Uhusiano wa China na nchi nyingi za Kiafrika ni wa kibiashara zaidi, ambapo China inalenga kugusa maisha ya Waafrika wengi wa kawaida kwa kutoa teknolojia na bidhaa za bei nafuu. Kwa upande mwingine, mkakati mpya wa Marekani kwa Afrika hauakisi sura ya kibiashara, na hauoneshi dalili za kugusa maslahi chanya ya moja kwa moja ya watu wa Afrika.

Hata hivyo, uhusiano kati ya Marekani na China na Marekani na Urusi hauwezi kuzorota kiasi cha kufikia kuzuka vita baina yao. Licha ya umbali wa kijiografia na uwezo mkubwa wa kijeshi ambao kila moja ya nchi hizo inajivunia, bado nchi hizo zinahusiana kiuchumi na hutegemeana kwa namna nyingi.

Pamoja na changamoto mbalimbali za hivi karibuni, China inafanya biashara zaidi na Marekani kuliko nchi nyingine yoyote duniani: uhusiano kati ya nchi ya Urusi na Marekani, au angalau uhusiano kati ya Rais Vladimir Putin na matajiri wengine wa Kirusi na Rais Donald Trump, umekuwa mzuri, mara nyingine hata kwa kuwabebesha mizigo mizito raia wa kawaida wa Marekani.

Utangamano huu unaleta ukakasi kwa uwezekano Marekani, China au Urusi kupigana vita kati yao, licha ya kudhihirika kwa dalili za mchuano zinazofanana na siasa zilizopelekea ukoloni barani Afrika ambapo wakati huo Ujerumani na Italia yalikuwa mataifa yenye nguvu yanayoibukia yakichuana na mataifa makubwa yaliyotawala dunia kama vile Uingereza na Ufarasa.

Kinyume na nadharia ya 'Mtego wa Thucydides' (Thucydides' Trap), ambayo inatabiri mapambano' ya ana kwa ana kati ya dola zinazoibukia na zile zilizopo, umbali wa kijiografia na mahusiano thabiti ya kibiashara yaliyopo kati ya Marekani, China na Urusi, kwa namna moja au nyingine, vinaondoa uwezekano wa mapambano ya kivita kutotokea kati yao kutokana na hasara kubwa kuliko faida watakayopata kutokana na vita.

Pia, jambo la muhimu zaidi, kukosa udhibiti kamili wa nchi yoyote ya Afrika pamoja na kiwango cha juu cha kujitambua barani humo, ambamo ndimo pangekuwa uwanja wa mapambano baina ya mataifa hayo makubwa, kunapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kanzisha vita vya kutumia wafuasi au mamluki barani humo licha ya kuwepo kwa migogoro ya ndani kwenye baadhi ya nchi barani Afrika.

Katikati ya sintofahamu hiyo, Afrika inapaswa kujifunza kuainisha vipaumbele vyake katika kushirikiana na nchi za kigeni na kufanya maamuzi ya mwelekeo na aina ya mahusiano kati yake na nchi yoyote bila kulazimishwa kudumbukia kwenye mtego wa propaganda nyepesi za kuipinga China ambazo zinachukulia siasa za kimataifa kwa mtizamo wa 'kupata' au 'kukosa' – kuchagua moja, ama nchi za Magharibi kwa upande mmoja au China na Urusi kwa upande mwingine.

Kutokana na kusosekana kwa mkakati wa utekelezaji wa wazi wa Mkakati wa Marekani kwa Afrika, bara hilo halina budi kufanya ushawishi ili kunufaisha watu wake ili isitokee hali ya kupata au kukosa, kushinda au kushindwa, bali wote kupata na kushinda kabla hali ya sasa haijawa mbaya zaidi.

*Francis Semwaza ni mshauri wa masuala ya mawasiliano ya maendeleo aliyepo Dar es Salaam, Tanzania. Baruapepe: frsemwaza@aol.com; Simu: 0716466044.

 

Suggset To Friend:   
Print